KAMISHENI YA ARDHI IMEPANGA KUYACHUKULIA HATUA MAENEO YOTE YALIYOTOLEWA NA SMZ KWA AJILI YA MAKAZI AMBAYO HAYAJAENDELEZWA

Na Maryam Nassor

KAMISHENI ya Ardhi Zanzibar imepanga kuyachukulia hatua maeneo yote yaliyotolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa wananchi kwa ajili ya makaazi, lakini hayajaendelezwa, kwa kuyarejesha serikalini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Kamisheni hiyo, Mlandege,  Unguja Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi, Mussa Kombo Bakar, amesema lengo la ziara yao ni kuyatembelea maeneo yote yaliyotolewa na Serikali ambayo bado hayajaendelezwa kwa matumizi ya makaazi.

Amesema kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Namba 12 ya mwaka 1992, mtu yeyote anayepewa ardhi kwa ajili ya makaazi anatakiwa kuiendeleza kwa mujibu wa sheria.

“Tumetoa muda wa miezi mitatu hadi Machi mwaka huu kwa wananchi kuyatembelea na kuyaendeleza maeneo waliyopewa. Endapo hayataendelezwa, yatarejeshwa serikalini,” amesema.

Aidha, amesema sheria hiyo inaelekeza kuwa ndani ya kipindi cha miaka miwili tangu kutolewa kwa kiwanja, mhusika anatakiwa awe ameshaanza au kukamilisha ujenzi, huku akibainisha kuwa bado kuna baadhi ya viwanja havijaendelezwa kwa zaidi ya miaka 20.

Amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haina nia ya kumuumiza mwananchi yeyote, kwani utaratibu huo ulielezwa wazi wakati wananchi wanapewa viwanja hivyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji, Said Salmini, amesema katika ziara hiyo hatua zitachukuliwa kwa wananchi waliotumia viwanja vya makaazi kinyume na makusudi, ikiwemo kujenga gereji au kuuza maeneo hayo.

Aidha, amewataka wananchi waliopewa maeneo hayo kutoziuza kwa wageni wasiokuwa wazanzibar, akisisitiza kuwa maeneo hayo yalikusudiwa kwa ajili ya wenyeji.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni hiyo alitangaza ratiba ya ziara hiyo, ambapo itaanza Machi 8 katika Wilaya ya Kusini Unguja na kukamilika Machi 30 mwaka huu katika Wilaya ya Mjini Unguja.

 

Top of Form

 

Bottom of Form


No comments

Powered by Blogger.