WAANDISHI WA HABARI NCHINI WAMEHIMIZWA KURIPOTI MATUKIO YA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA VIJIJINI.
Na Maryam Nassor
Waandishi wa habari
nchini wametakiwa kuibua na kuripoti matukio ya udhalilishaji wa kijinsia
yanayowakumba wanawake na wasichana, hususan katika maeneo ya vijijini ambako
bado kuna mwamko mdogo wa kuripoti vitendo hivyo.
Wito huo umetolewa na
Mjumbe wa Bodi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar
(TAMWA ZNZ), Bi. Hawra Shamte, katika mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa
chama hicho, Tunguu, Unguja.
Amesema matukio ya
udhalilishaji wa kijinsia yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku, hasa katika
maeneo ya vijijini ambako wananchi wengi hushindwa kuripoti matukio hayo na
hivyo kutokuchukuliwa hatua stahiki.
“Waandishi wa habari mna
jukumu kubwa la kuibua na kuripoti matendo haya, yakiwemo mauaji na vitendo vya
udhalilishaji, ili jamii iweze kupata uelewa na kuchukua hatua sahihi,” amesema
Bi. Shamte.
Amefafanua kuwa, baadhi ya vitendo wanavyofanyiwa wanawake na wasichana ni pamoja na kushikwa sehemu za miili yao wakiwa kwenye vyombo vya usafiri, pamoja na kuibiwa mali zao hata na baadhi ya waume zao.
Kwa upande wake, Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka TAMWA ZNZ, Mohamed Khatib, amesema waandishi wa habari wana wajibu wa kuelimisha jamii kuhusu haki zao na kufuatilia kesi za udhalilishaji hadi mwisho ili kuhakikisha haki inapatikana.“Ni jukumu lenu
waandishi wa habari kuripoti matendo ya udhalilishaji kwa wanawake na wasichana
ili kujenga jamii salama,” amesema Khatib.
Naye Afisa Programu wa TAMWA ZNZ, Asya Hakim, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ‘Tunaweza Pamoja Kumaliza Udhalilishaji wa Kijinsia Dhidi ya Wanawake na Wasichana’, unaotekelezwa katika mikoa miwili ya Zanzibar—Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba.
Amesema lengo la mradi
huo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari pamoja na wadau wengine ili
kusaidia kupunguza na hatimaye kumaliza matukio ya udhalilishaji wa kijinsia.
Ameongeza kuwa ,mradi
huo unatekelezwa katika maeneo yenye matukio mengi ya udhalilishaji, ikiwemo
maeneo ya usafirishaji, masoko na sehemu za kukaushia dagaa, ambako wanawake na
wasichana hukumbana na vitendo hivyo mara kwa mara.
Baadhi ya waandishi wa
habari walioshiriki mafunzo hayo kutoka Asalam FM na Zenji Post Blog wamesema
mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi na kuripoti kwa
ufanisi zaidi masuala ya kijamii.
Mafunzo hayo ya siku mbili yametolewa kwa waandishi 20 kutoka vyombo mbalimbali vya habari Zanzibar chini ya mradi wa Pamoja Tunaweza unaotekelezwa na TAMWA ZNZ, kwa lengo la kuendelea kuibua na kupambana na vitendo vya udhalilishaji hasa vijijini.
Post a Comment