WANAWAKE WAMETAKIWA KUTUMIA MAFUNZO KUIMARISHA USHIRIKI WAO KATIKA UONGOZI
Na Maryam Nassor
VIONGOZI wanawake wametakiwa kutumia ipasavyo maarifa na
ujuzi wanaoupata kupitia mafunzo ya mradi wa W-LEAD ili kutimiza ndoto zao za
kiuongozi na kuongeza ushiriki wao katika nafasi mbali mbali za uongozi.
Wito huo umetolewa na Afisa Tathmini na Ufuatiliaji Mohamed Khatib Mohamed kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ) akimuakilisha
Mkurugenzi wa chama hicho Nairat Abdulah , wakati wa ufunguzi wa mafunzo
ya siku nne kwa viongozi wanawake vijana kutoka vyama vya siasa, asasi za
kiraia na vyuo vikuu Zanzibar yaliyofanyika katika Afisi za TAMWA Tunguu
Unguja.
Amesema, lengo la
mafunzo hayo ni kuwawezesha wanawake kuelewa masuala ya uongozi, kujiamini na kupata ujuzi utakaowawezesha
kushiriki kikamilifu katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Amesema kupitia mradi huo katika awamu
ya pili , TAMWA-ZNZ inalenga kuwajengea uwezo wanawake wengi ili waweze kuingia
katika nafasi za uongozi, huku ikipanga kuwafikia vijana 50, wakiwemo 30 kutoka
Unguja na 20 kutoka Pemba.
Ameeleza kuwa TAMWA-ZNZ inatekeleza mradi huo kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo Jumuiya ya Watu Wasioona Zanzibar
(ZANAB), Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Zanzibar
(ZU), kwa lengo la kuhakikisha washiriki wanapata maarifa na ujuzi unaohitajika
katika kuimarisha uwezo wao wa kiuongozi.
“Lengo kubwa ni kuona mnapomaliza mafunzo haya mnaenda
kutekeleza yale mliyofundishwa na kuelekezwa, ili siku moja tusikie kuwa
miongoni mwenu wametoka viongozi mbalimbali wanaoweza kugombea nafasi tofauti
za uongozi,” amesema Mohamed.
Amesema kuwa, mafunzo hayo ni awamu ya pili ya mradi huo,
ambapo baada ya kukamilika kwa mafunzo, washiriki wanatarajiwa kwenda
kuyafanyia kazi maarifa waliyopata.
Ameongeza kuwa, miongoni mwa washiriki hao watachaguliwa
vijana 20 waliofanya vizuri ambao watapata fursa ya kwenda kujifunza kwa
vitendo katika taasisi mbalimbali, hatua inayolenga kuwapa uzoefu zaidi katika
masuala ya uongozi.
Aidha, amewataka viongozi hao vijana kujiamini, kutumia fursa wanazopata na kuwa na dhamira ya kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi ili kutimiza ndoto zao.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa TAMWA-ZNZ, Sophia
Ngalapi, amewataka viongozi wanawake kutumia mafunzo hayo kuongeza maarifa, kujiamini
na kujiandaa kushiriki kikamilifu katika kugombea nafasi za uongozi.
Akizungumzia manufaa ya mafunzo hayo, Nafda Ali Hassan,
mshiriki kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema mafunzo hayo yatamsaidia
kuongeza kujiamini na kuimarisha uwezo wake wa kiuongozi.
Amesema atatumia maarifa atakayoyapata kuwafikia
wanawake wengine na kuwajengea uwezo wa kiuongozi ili nao waweze kutimiza ndoto
zao.
Naye Khadija Anuwar Mohamed, kutoka Chama cha ACT
Wazalendo, ameishukuru TAMWA-ZNZ kwa kutoa mafunzo hayo, akisema yamempa
ujasiri na imani kuwa anaweza kushika nafasi za uongozi.
Amesema uwepo wa wanawake wengi katika nafasi za uongozi
umekuwa chachu kwa wanawake wengine kujiamini na kuona kuwa wanaweza kushiriki
katika michakato ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Kwa upande wake, Lulu Alawi Abdallah, kutoka Jumuiya ya
Viziwi Zanzibar (JUVIZA), amesema mafunzo hayo yatamsaidia katika safari yake
ya kutimiza ndoto yake ya kuwa kiongozi.
Amesema mafunzo hayo ni fursa muhimu ya kuongeza uelewa na uwezo wa wanawake wenye ulemavu kushiriki katika uongozi na kutoa mchango wao katika maendeleo ya jamii.
Mafunzo hayo ya siku nne yameandaliwa na TAMWA-ZNZ kwa kuwashirikisha
viongozi wanawake kutoka taasisi mbalimbali, zikiwemo JUWAUZA, ZANAB, JUVIZA,
vyuo vikuu Zanzibar na vyama vya siasa, kwa lengo la kuwajengea uwezo,
kuimarisha kujiamini na kuongeza ushiriki wao katika nafasi za uongozi.


Post a Comment