RUFAA YAKATALIWA' JAJI AMURU MSHITAKIWA KUTUMIKIA KIFUNGO CHA MIAKA 10 JELA'

 

 


NA MARYAM NASSOR PEMBA,                                         HUKUMU ya rufaa iliyokatwa mahakama kuu Zanzibar, kanda ya Pemba imekataliwa na Jaji wa mahakama hiyo, kutokana na upande wa mashtaka kufanikiwa kuthibitisha kosa pasi na shaka yoyote,na kuamuru mshtakiwa wa kesi hiyo,Zuber Jerad Said wa Bopwe Pemba, kutumikia kifungo , cha miaka 10 jela,kwa kosa la kupatikana na kete 1678 za dawa za kulevya..

Akisoma hukumu hiyo , Jaji wa mahakama hiyo Ibrahim Mzee Ibrahim alisema kuwa, rufaa hiyo imekataliwa kutokana na kuwa  upande wa mashtaka walikuwa na mashahidi ambao walitoa ushahidi wa wazi na wakuaminika hivyo ,wao hawawezi kubatilisha hukumu hiyo.

Jaji huyo, alisema kuwa ,mshtakiwa  alikamatwa na pw3 na pw4 akiwa na kielelezo , ambacho ni mfuko wa dawa za kulevya aina ya heroin kete  1678  zenye uzito wa  41.53g.

 Alieleza kuwa , wakili wa utetezi Abeid Mohamed Said  wakati anaomba rufaa, aliieleza mahakama  sababu ya rufaa, kuwa mteja wake,  hakupatiwa haki kutokana na  ushahidi uliyotolewa na kumtia hatiani haukufikia kiwango au ulichezewa.

Wakili wa utetezi alisema, ukamatwaji wa mteja wake, haukufuata sheria na ulikuwa kinyume na kifungu  cha 35 (1) (4) cha sheria namba7 ya mwaka 2018.

Alisema kuwa, mteja wake alikamatwa hazarani na askari waliokuwa kwenye doria, lakini hawakuita shahidi  huru hata mmoja ili kushuhudia kitendo hicho, hivyo inaoneshaa polisi hao walikuwa na nia mbaya.

“Mteja wangu alikamatwa hazarani  na Polisi waliyokuwa doria, lakini baada ya kumkamata  hawakuita shahidi huru ambae angeshuhudia tukio hiyo” alisema wakili huyo.

 Aidha, alisema kuwa,pia mnyororo wa kesi ulikatika, hiyo inathibitishwa na pw3 na pw4 ,kwani kulikuwa hakuna ushahidi wa maelezo wapi kielelezo hicho kilihifadhiwa,  mara baada ya kufikishwa kituoni.

Hivyo, kwa mantiki hiyo, wakili Abeid, aliiomba mahakama hiyo ,itupilie mbali  hukumu hiyo, adhabu ibatilishwe na mteja wake achiwe huru.

Akijibu, tuhuma hizo mwendesha mashtaka wa Serikali , alisema kuwa ni kweli mshtakiwa alikamatwa hazarani lakini ilikuwa ni wakati wa usiku  majira ya saa 4,hivyo kama tunavyojua mazingira ya Pemba barabarani huwa hakuna watu wengi wanaotembea.

Alisema kuwa, muomba rufaa huyo,  ushahidi ulimtia hatiani moja kwa moja kutokana na kuwa alikamatwa na mfuko wa kete 1678, aliyokuwa kautia ndani ya fulana yake.

Aidha Dpp huyo, alisema kuwa, mnyonyoro wa kesi haukukatika,  mara baada ya mtuhumiwa kukamatwa na kufikishwa Polisi pamoja na kielelezo chake, alikabidhiwa askari aliyekuwepo na ilipofika asubuhi kielelezo hicho alikabidhiwa mtunza vielelezo na kupewa namba WIR2008/2021, hadi kilipokuja kuchukuliwa na askari mpelelezi ili kukipeleka maabara.

Alisema, kuhusiana na kukiukwa kwa kifungu cha 35(4) cha sheria namba 7 ya mwaka 2018 ,alisema kifungu hicho hakija kiukwa kwani mara nyengine si lazima kufuatwa kwa kifungu hicho haswa kutokana na mtuhumiwa hakubainisha ni watu wapi wapewe taarifa, kuwa yeye yupo kituoni.

 Baada ya kuupitia ushahidi huo, Jaji Ibrahim alisema  kuwa ameupitiwa kwa makini  ushahidi huo na kujiridhisha, kwa kuona upande wa mashtaka  ulifanikiwa kusibitisha tuhuma hizo pasi na shaka kwani,  ulikuwa na  nafasi nzuri ya kuwaona mashahidi katika mazingira hayo,na ulionesha kuwa mnyororo wa kesi haukuatika  na kifungu cha  35 (4) cha sheria namba 7 ya mwaka 2018 hakikukiukwa.

Kwa mantiki hiyo,  rufaa hiyo imekataliwa na mshtakiwa anatakiwa kutumikia kifungo chake cha miaka 10 jela alichohukumiwa na mahakama ya Mkoa.

Awali shauri hilo lilifunguliwa june 16, mwaka  2021 katika mahakama ya mkoa na mshtakiwa alikuwa ni Zubeir Jerad Said (30) mkaazi wa Bopwe  wilaya ya wete Pemba.

Ilidaiwa kuwa, siku ya tarehe 6/6/2021 huko Bopwe majira ya saa 4:00 usiku bila ya halali,mshitakiwa huyo  alipatikana na kete 1678  zenye uzito wa  41,53g jambo ambalo ni kosa kisheria.

Kupatikana na madawa ya kulevya, ni kinyume na kifungu cha 21 (1) (d)cha sheria za mamlaka ya  kudhibiti  na kupambana na dawa za kulevya  Zanzibar, cha sheria namba 8 ya mwaka 2021 sheria za Zanzibar.

No comments

Powered by Blogger.