TAMWA ZNZ Yasisitiza Uwezeshaji wa Wanawake ni Msingi wa Usawa.



NA MARYAM NASSOR

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ) kimesema kwa muda mrefu wanawake wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi katika kushiriki uongozi wa kisiasa, zikiwemo mifumo dume, mila na desturi ambazo zimekuwa zikichangia kuwanyima fursa za uongozi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa chama hicho, Nairat Abdullah, katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa TAMWA, Tunguu, Unguja.

Amesema, kumuwezesha mwanamke ni msingi wa kujenga jamii imara yenye haki na usawa kwa wote .

Aidha, amesema kuwa licha ya changamoto zilizopo, kwa miaka ya hivi karibuni kuna mwanga wa matumaini, ambapo uelewa na ujasiri wa wanawake kushiriki katika siasa na uongozi umeongezeka, hali inayowafanya wengi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Ameeleza kuwa, mfano mzuri ni uchaguzi wa mwaka 2025 ambapo, kwa mara ya kwanza katika historia ya Zanzibar, wanawake wamejitokeza kugombea nafasi ya urais, jambo ambalo ni hatua kubwa na ya kihistoria.

“Tunawapongeza wanawake wote waliothubutu kujitokeza, akiwemo Bi. Laila Rajab Khamis ambaye aliteuliwa rasmi kugombea nafasi hiyo kupitia chama cha NCCR Mageuzi,” amesema Mkurugenzi huyo.

Ameongeza kuwa, jumla ya wanawake 809 walishiriki katika chaguzi za ndani za vyama, huku wanawake 324 wakiteuliwa kugombea nafasi mbalimbali Zanzibar, jambo linaloonesha jitihada na dhamira ya wanawake kushiriki kikami,ifu katika uongozi

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Norway nchini Tanzania, Anette Otiliee, amesema wataendelea kuunga mkono jitihada za usawa wa kijinsia, ikiwemo afya na haki za uzazi, akieleza kuwa bila hayo wanawake hawawezi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii.

“Tutaendelea kushirikiana na wadau kama ninyi mnaoweza kubadilisha ahadi kuwa matokeo halisi,” amesema.

Ameeleza kuwa, wanawake bado wanakumbana na ubaguzi na vitendo vya ukatili, changamoto ambazo ni za kimfumo na zinahitaji suluhisho la pamoja ili kupatikana maendeleo endelevu.

“Norway inajivunia kusimama pamoja na TAMWA katika kazi hii, na tutaendelea kuunga mkono usawa wa kijinsia,” ameongeza.

Naye Mjumbe wa Bodi ya TAMWA ZNZ, Bi. Hawra Shamte, amesema jitihada za taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine zimeanza kuleta mabadiliko chanya.

Amesema, kupitia jitihada hizo, wanawake wengi wamepata uelewa na ujasiri wa kushiriki katika siasa na uongozi.

Kwa upande wake, Afisa Habari wa TAMWA, Khairat Haji, amesema kupitia tathmini iliyofanywa na TAMWA ZNZ, jamii imeonesha mwitikio mzuri kwa uongozi wa wanawake.

Amefafanua kuwa, wanawake 132 walihojiwa, ambapo asilimia 96 walionesha kuwa na uelewa kuhusu uongozi wa wanawake, huku asilimia 68 wakisema uongozi wa wanawake unafanya vizuri na kuleta mabadiliko katika jamii.

Washiriki mbalimbali pia walitoa maoni na ushuhuda kuhusu safari ya wanawake katika uongozi. Naima Salum Hamad amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado wanawake wanahitaji kushikamana na kusaidiana.

Naye, Rehema Khamis kutoka Dawati la Jinsia katika Chuo Kikuu cha SUZA amesema bado kuna changamoto ya baadhi ya wanawake kutoshirikiana katika siasa, na kusisitiza umuhimu wa kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi pamoja na kuwawezesha kiuchumi.

Maadhimisho hayo yalifanyika kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali ikiwemo TAMWA ZNZ, ZAFELA, PEGAO, JUWAUZA, PYI na CRDB Bank, chini ya ufadhili wa Norway, yakiwa na kaulimbiu isemayo: “Haki, usawa na kuchukua hatua kwa wanawake na wasichana.”

                                  Mwisho

Top of Form

Bottom of Form

 

No comments

Powered by Blogger.